Jumatatu, 16 Septemba 2013

Obama awasiliana na rais mpya wa Iran

Obama akizungumza juu ya Iran 

Rais Obama anasema ameandikiana barua na rais mpya wa Iran, Hasan Rouhani.
Akihojiwa na televisheni ya Marekani, ABC, Obama alisema Iran inafahamu kuwa sera ya Iran ya kujaribu kuunda silaha za nyuklia ni swala kubwa zaidi kwa Marekani kushinda silaha za kemikali zilizotumiwa na Syria.
Rais Obama ametokeza mara nyingi kwenye televisheni za Marekani katika wiki za karibuni kuwakumbusha watu tishio la silaha za kemikali za Syria.
Jumapili aliulizwa jee Iran itafikiria vipi msuko-suko wa Syria?.
Rais Obama alisema amewasiliana na rais mpya wa Iran, Bwana Rouhani.
Na alisema kuna tofauti baina ya Iran na Syria.
Alikiri kuwa mradi wa nyuklia wa Iran unavotishia Israel, ni jambo lililo karibu na masilahi ya Marekani kushinda silaha za kemikali.
Aliongeza kusema kuwa mashindano ya kumiliki silaha za nyuklia yanaweza kutibua sana eneo hilo.
Akilinganisha Iran na Syria, Rais Obama alisema anafikiri Iran inatambua kwamba kuna njia ya kusuluhisha maswala haya kidiplomasia, ingawa alikiri kuwa ni vigumu kuzungumza na Iran.


Uchaguzi wa wabunge wafanyika Rwanda

 

Raia wa Rwanda milioni sita leo wanapiga kura kuwachagua wabunge katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Rwanda inasifika sana kwa kuwa na wanamama wengi kwenye nyadhifa za uongozi wa kitaifa.
Uchaguzi huu usio na upinzani mkubwa ni kama kupiga muhuri tu uongozi wa chama cha RPF chake Rais Paul Kagame ambacho kimekuwa uongozini tangu kumalizika kwa mauaji ya Kimbari mwaka 1994.

Mayweather adhihirisha ubingwa wake

 

Floyd Mayweather ameboresha umaarufu wake kama bingwa wa masumbwi baada ya kumshinda Saul Alvarez mjini Las Vegas.
Ushindi wa Mayweather mwenye umri wa miaka 36, umempa taji la WBC na WBA uzani wa kati. Pia ameshinda katika michuano yote 45 aliyopigana kama mwanamasumbwi wa kulipwa.

Arsenal yatembeza kichapo

Arsenal watamba 

Aaron Ramsey alishinda magoli 2 na kuiwezesha timu yake kuinyoa Sunderland 3-1 huku meneja Paolo Di Canio akipewa kadi nyekundu.
Goli la kwanza lilipatikana baada ya juhudi za mchezaji mpya aliyesajiliwa na Arsenal Mesut Ozil ambaye alimwandalia pasi murua Olivier Giroud aliyenusa nyavu.
Goli hilo lilisawazishwa na Craig Gardner muda mfupi baada ya mapumziko.

Magoli mengine mawili ya Arsenal yalitiwa kimiani na Ramsey na kuiwezesha timu yake kuandikisha ushindi wa mabao 3-1 ambao ni wa tano mfululizo.