Jumamosi, 4 Januari 2014

Mkwasa achimba mkwara jangwani!!

Kocha Charles Mkwasa akionyesha wachezaji wake namna ya kutuliza mpira.
Kwa ufupi
  • Yanga ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 29, ikifuatiwa na Azam na Mbeya City zenye pointi 28 kila moja.
  • Mkwasa na Pondamali waliwahi  kuwa wachezaji wa Yanga  na wamepewa jukumu la kuwa wasaidizi, huku uongozi wa klabu hiyo ukiendelea na harakati za kutafuta kocha mkuu kutoka barani Ulaya, atakayekuja kurithi mikoba ya Kocha Ernest Brandts na hadi sasa ni zaidi ya makocha 45 wameomba kuchukua jukumu hilo. 
Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa jana alianza kazi rasmi ya kukinoa kikosi hicho na kusisitiza kuwa mchezaji asiyekuwa na nidhamu hana nafasi katika timu yake.
Mkwasa aliyekuwa kocha mkuu wa Ruvu Shooting  amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha Yanga akichukua jukumu la kuwa kocha msaidizi.
Hata hivyo, kwa sasa Mkwasa atatekeleza majukumu yake akiwa kaimu kocha mkuu wa Yanga akirithi nafasi iliyoachwa wazi na Ernest Brandts alifungashiwa virago hivi karibuni sambamba na benchi zima la ufundi la timu hiyo.
Akizungumza baada ya mazoezi ya kikosi chake jana asubuhi Mkwasa alisema, hatakuwa tayari kutoa nafasi kwa mchezaji wake yeyote kumtawala kwani endapo ataruhusu hali hiyo timu itakosa nidhamu. 
“Kimsingi Yanga ina wachezaji wazuri ingawa  wanahitaji stamina ya kutosha na ndicho kitu ambacho nimeanza nacho leo na baada ya hapo tutaendelea na vitu vingine.
“Isipokuwa nasisitiza nidhamu kwangu ndiyo kila kitu ili timu iweze kufanya vizuri na nitatilia mkazo hilo, mchezaji ambaye hatakuwa tayari kufuata taratibu zilizowekwa ajue hana nafasi kwangu,” alisema Mkwasa.
Katika mazoezi hayo yaliyodumu kwa  saa 2:15, mwandishi wa gazeti hili aliwashuhudia wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi ya kukimbia, viungo na namna ya kukokota mpira na kupiga mashuti.
Kwa upande wake, kocha mpya wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali ambaye kama ilivyo kwa Mkwasa alianza  kibarua chake jana alisema:”Nilikuwa na progamu 12 za mazoezi, lakini makipa wangu wamenilalamikia kwamba uwanja ni mbovu hivyo nimelazimika kuishia programu nane.
“Pamoja na hayo nimewaambia hivi ndivyo viwanja vyetu wanatakiwa wakubaliane na hali halisi maana  sitaweza kuharibu programu zangu kwa sababu ya uwanja.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni